Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ametaja hatua saba ambazo Serikali yake imeanza kuzichukua ama inakusudia kuzichukua ili kukabiliana na msongamano wa magari katika Jiji la Dar Es Salaam.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa msongamano wa magari ni ishara ya ubora wa maisha ya wananchi na ustawi wa Watanzania kwa sababu miaka 20 ama hata 10 iliyopita, Jiji la Dar Es Salaam halikuwa na msongamano.
Hata hivyo, Rais Kikwete ameonya kuwa, kama ilivyo katika miji yote mikubwa duniani, ni jambo lisilowezekana kumaliza tatizo la msongamano wa magari katikati ya Jiji la Dar Es Sslaam (Central Business District), hasa kwa kutilia maanani kuwa hakuna shaka kuwa watu wataendelea kununua magari na huwezi kuvunja nyumba zote katikati ya Jiji ili kupanua barabara.
Rais Kikwete ameyasema hayo , wakati akizindua rasmi Barabara kisasa ya Mwenge -Tegeta kwenye Barabara ya New Bagamoyo Road. amezitaja hatua hizo za kukabiliana na msongamano wa magari katika Mji wa Dar Es Salaam kuwa ni pamoja na ujenzi wa njia ya Mabasi Yaendayo Kasi (DART), ambao awamu yake ya kwanza inakaribia kukamilika pamoja na uanzishwaji wa huduma za kisasa za usafiri wa treni katika maeneo mbali mbali ya jiji hilo.
Hatua ya tatu ambayo Rais Kikwete ameitaja ni kujengwa kwa barabara za juu kwa juu (flyovers) katika maeneo ya TAZARA na Ubungo, yenye msongamano wa watu wengi, na ujenzi wa barabara 12 za kuzunguka Jiji (Ring Roads) na nyingine za kuunganisha maeneo ya jiji hilo kama vile upanuzi wa Barabara ya Uhuru kuwa njia mbili kila upande badala ya njia moja ya sasa.
Aidha, Rais Kikwete amezitaja hatua nyingine kuwa ni ujenzi wa Daraja jipya la Salender ambalo litapitia baharini, usafiri wa kivuko kipya kutoka Bagamoyo hadi Dar Es Salaam na ujenzi wa miji midogo ya kisasa inayojitegemea katika maeneo ya Kigamboni, Mabwepande na Luguruni.
Rais Kikwete amesema kuwa baadhi ya hatua hizo zinazochukuliwa ama zinalengwa kuchukuliwa na Serikali zimekuwa zinakabiliwa na siasa nyingi za kupinga miradi hiyo kutoka kwa baadhi ya viongozi na wanasiasa nchini ambao amewaita “watu wenye upeo mfupi”.
Akizungumza wakati wa akizindua rasmi Barabara ya Kisasa ya Mwenge-Tegeta ambayo ni sehemu ya Barabara ya New Bagamoyo Road, mjini Dar Es Salaam iliyo na urefu wa kilomita 12.9 imegharimu kiasi cha Sh. bilioni 77.85, fedha ambazo zimetolewa na Serikali ya Japan kupitia Shirika lake la Maendeleo ya Kimataifa la JICA. Serikali ya Tanzania imechangia asilimia 7.64 katika gharama za ujenzi wa Barabara hiyo.
Rais Kikwete amefanya uzinduzi huo katika eneo la Makutano ya Kambi ya Jeshi ya Lugalo na Barabara ya Kawe katika sherehe iliyoshuhudiwa na mamia ya wananchi. Alikuwa ni Rais Kikwete ambaye aliweke jiwe la msingi la ujenzi wa Barabara hiyo Aprili 4, mwaka 2011.
Barabara hiyo ni awamu ya kwanza ya ujenzi wa Barabara itokayo Makutano ya Barabara ya Kawawa, Kinondoni hadi Tegeta. Ujenzi wa awamu ya pili wa kilomita 4.3 kati ya Mwenge na Makutano ya Barabara ya Kawawa, unatarajiwa kuanza wakati wowote baada ya mipango yote ya ujenzi huo kukamilika.
Barabara hiyo ya Mwenge-Tegeta inalenga kupunguza msongamano wa magari katika eneo la kaskazini mwa Dar Es Salaam na pia ni sehemu ya bararaba kuu inayounganisha Jiji la Dar Es Salaam na Mkoa wa Pwani, kupitia Wilaya ya Bagamoyo, na kuunganisha mikoa hiyo na mikoa ya kaskazini mwa Tanzania.
Akizungumza kwenye sherehe hiyo ya uzinduzi wa Barabara hiyo iliyojengwa na Kampuni ya Konoike kutoka pia Japan, Balozi wa Japan katika Tanzania, Mheshimiwa Masaki Okada amesema kuwa ujenzi wa barabara hiyo ulichelewa kukamilika mwaka jana, kama ilivyopangwa, kwa sababu ya wajenzi kukabiliwa na matatizo ya mafuriko makubwa yaliyotokea mwaka 2011.
Mbali na kutaja misaada mingi katika sekta ya miundombinu na hasa barabara ambayo imefadhiliwa na Japan katika miaka mingi iliyopita, Mheshimiwa Okada amesema kuwa Japan sasa iko tayari kuanza ujenzi wa Barabara ya Gerezani-Bendera Tatu, Dar Es Salaam, utakaogharimu Sh. bilioni 18.5, msaada kutoka Japan.
Aidha, Balozi huyo amewaomba radhi Watanzania kutokana na ucheleweshaji wa kuanza kwa ujenzi wa barabara ya juu kwa juu –flyover- katika eneo la TAZARA, Dar Es Salaam, ambao utagharimu Sh. bilioni 53 ambazo zinatolewa na Serikali ya Japan kupitia Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la JICA.
Amesema kuwa ujenzi huo umechelewa kwa sababu makandarasi wa Kijapan ambao walitakiwa kujengaflyover hiyo wanakabiliwa na kazi nyingi huko nyumbani za kujenga upya miundombinu iliyoharibiwa na tetemeko na kimbunga cha Great East Japan Earthquake and Tsunami, kilichotokea Machi 2011 na kusababisha uharibifu mkubwa mno.
Aidha, amesema kuwa wajenzi hao pia wanalazimika kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha miundombinu ya kuiwezesha Japan kuandaa Michezo ya Olimpiki ambayo imepangwa kufanyika nchini humo mwaka 2020.
No comments
Post a Comment